LEO NAONGELEA NENO "FURSA"(OPPORTUNITY).
Nikuombe unifuatilie maana nina uhakika utapata kitu mwishoni na hautabaki kama ulivyo kuwa.
Nina ongea na watu wote lakini hasa ujumbe wangu uwafikie wana Dodoma ambao michango yao ya juma lililopita katika kipindi cha "Malumbano ya hoja "Kinachoendeshwa na kurushwa na runinga ya ITV imenishawishi nami nitoe mtazamo wangu kuhusu FURSA.
KARIBU :
Miaka minne (4) iliyopita niliandika makala ambayo nilikuwa nataja maeneo sita (6)ya uwekezaji wa Mungu kwa mtu yeyote ili yamsaidie kufikia mafanikio yake.FURSA nililitaja kama miongoni mwa maeneo hayo.
Sasa tafsiri ya FURSA ni ipi kwa mujibu wangu?
"Fursa" Ni kitu chochote ambacho ukikitendea kazi au kukitekeleza katika wakati sahihi ,kinakupa matokeo au manufaa chanya. Hapa naomba upigie mstari neno "WAKATI SAHIHI"halafu fuatana nami utanielewa nitakapokutajia sifa au tabia za Fursa.
FURSA siyo BIASHARA, KAZI, NAFASI/CHEO/MADARAKA,AJIRA, KUJIAJIRI n. k kama wengi mnavyodhani ama kuitafsiri fursa, hapana. Hivyo vyote ni MATOKEO ya fursa .UBUNIFU pia siyo tafsiri sahihi ya fursa. Isipokuwa ubunifu ni hitaji au eneo mojawapo la kuifanya Fursa ikupe matokeo sawa sawa na thamani ya fursa hiyo.
VYANZO /VICHOCHEO VYA FURSA :Ni pamoja na :
1:Uwepo wa Tatizo Mahali -Mtu akibaini kuwepo kwa tatizo mahali na akawaza kuja na suluhisho huyo atakuwa ameiona fursa. Na hivyo hapo fursa siyo suluhisho alilokuja nalo bali TATIZO.
2:Uhitaji-Kunapokuwepo na uhitaji wa kitu chochote mahali hiyo ni fursa.
3:Nafasi -Nafasi uliyonayo mahali pia unaweza kuitumia kama fursa ukaitumia kukupa unachokitaka na ukanufaika na wewe kuwa katika nafasi hiyo.
4:Kipaji/Kipawa/Karama ulicho nacho -hiyo pia ni fursa kwako.
5:Uwezo binafsi(inborn ability) ulionao-Hiyo ni fursa kwako. Unaweza ukawa na uwezo mzuri wa kuongea mbele za watu jambo ambalo wengine hawawezi. Hiyo ni fursa kwako. Itumie. Ndiyo maana licha ya kwamba tunasema wote lakini si kila mtu anaweza kuwa MC.
6:Elimu/Weledi/Ufahamu ulionao -Hiyo ni fursa pia.
7:Mahusiano/Connections ulizonazo na watu wanaokuzunguka -Hiyo ni fursa pia itumie. Usipoitumia watu watakutumia wewe kuipata au kuitumia hiyo fursa ya mahusiano uliyonayo.Usinishangae,watu watakufanya ngazi au daraja la wewe kufanikisha mambo hayo na wewe kuachwa doro.
SIFA /TABIA ZA FURSA.
1:IPO KILA MAHALI -Yaani hata hapo ulipo unalalamika maisha magumu lakini akija mwingine mwenye jicho la kuiona na kuitafsiri fursa katika matendo anatoboa na kukuacha unashangaa. Tatizo siyo fursa ila jicho na uwezo wa kuona na kuitambua kwa kuitafsiri Kama hii ni fursa.
2:HAIBISHI HODI -fursa inapokuja haibishi hodi wala kuwa na viashiria vya moja kwa moja. Unahitaji jicho lenye usikivu makini kuibaini. Rejea namba moja hapo juu.
3:KUZALISHA MAHITAJI-Fursa inapokuwepo mahali ina tabia ya kuzalisha mahitaji ambapo watu wengine huchanganya Kati ya mahitaji na fursa. Fursa inaweza kuwa moja tu lakini ikazalisha mahitaji lukuki. Ambapo katika uhalisia kinachonufaisha ni hayo mahitaji siyo fursa yenyewe.
4:KUZALISHA FURSA ZINGINE -fursa inapokuja inatabia ya kuzaa fursa nyingine. Kwa mfano wawekezaji wanaweza kuja kuchimba madini mahali ,hiyo ni fursa, lakini fursa hiyo inaweza kuzaa fursa ya uwepo wa barabara n. k
5:INA TABIA YA KUISHA THAMANI KATIKA MUDA WA KUDUMU/KUWEPO- usishituke, kwani hujawahi kusikia mtu anakwambia "Changamkia Fursa" Tafsiri yake hapo ni kwamba ukizubaa siyo nafasi zitajaa, hapana ila wakati utakapokuwa tayari, tayari muda wa uhai wa fursa hiyo utakuwa umekwisha. Kwa lugha nyepesi ,fursa itakuwa ime expire katika Muda. Nisikilize vizuri, sijasema itakuwa ime expire katika matumizi ila nimesena muda. Nisikikize.. Matumizi kuwa hai haimanishi na muda uko hai. Matumizi ya mpira miguuni yanaweza kuwa hai lakini muda usiwe hai kwa mchezaji. Hujasikia watu wakisema Mwili unataka ila muda unakataa? Nadhani umeelewa.
Sasa nikueleze
VITU /MAMBO YA KUZINGATIA KUYAFANYA ILI KUIFANYA FURSA IKUPE MATOKEO/MANUFAA CHANYA. (hapa ni muhimu Sana)
1:UWEZO/JICHO LA KUIONA NA KUITAMBUA KAMA HII IN FURSA. -kumbuka nimekwambia fursa haibishi hodi kukuashiria kwamba nipo hapa. Hivyo unahitaji uwezo wenye utulivu na jicho lenye masikio ya kuitafsiri hali flani kuwa ni fursa kwako. Ndiyo maana fursa ziko kila mahali kakini wanaoziona ni wachache.
2:UWEZO WA KUJUA KINA(TA)AMBATANA NA FURSA HIYO. naomba tuelewane Kwamba,kinachoambatana na fursa siyo mahitaji ya fursa. Mahitaji ya fursa hutokana na kiambatanisho cha fursa. Kwa mfano ikitokea fursa ya eneo flani kujengewa hospitali, kiambatanisho cha hiyo fursa kinaweza kuwa miundombinu ikiwemo majengo, barabara n. k.
Hayo siyo mahitaji, ni viambata. Mahitaji ni vile vitu vitakavyohitajika III hiyo miundombinu ya majengo na barabara viwepo. Sijui Kama unanielewa. Mungu akusaidie.
3:MAHITAJI YA FURSA HIYO -lazima uwe na uwezo wa kufahamu na kuainisha mahitaji ya ujio wa fursa hiyo. Kwa mfano fursa ya ujenzi mahitaji yake ni pamoja na vifaa vya ujenzi. Mabati, nondo, tifali, saruji n. k.
4:Hili ni eneo muhimu sana katika kuifanya fursa ikupe matokeo. Eneo hili linaitwa
KUIPA THAMANI YA ZIADA FURSA (kwa kifupi Mimi naliita -UBUNIFU)
ubunifu katika fursa ni jambo muhimu sana. Kwa nini?
Unapowekeza katika ubunifu katika kuifanya fursa ikupe matokeo, maana yake ni kwamba unaiwekee mazingira fursa hiyo ikupe matokeo makubwa zaidi. Ubunifu unaleta utofauti wa kitu. Ubunifu unaweza kuwa katika eneo la ubora, kiwango au namna ya kuitangaza fursa.
Ngoja nitoe mfano kidogo hapa III unielewe.
Ubunifu kwa mfano katika dunia ya sasa iliyojaa ushindani wa soko, kwa mfano wewe unajenga nyumba za kupangisha wafanyakazi ama watu wa daraja flani la Kati au la juu. Badala ya kuishia kujenga nyumba nzuri tu kwa muonekano unaweza ukaenda mbali zaidi madhali wanaokuja kupanga wana uwezo, wewe ukajenga zile nyumba halafu ukafunga na mifumo ya ulinzi ya kielektroniki na teknolojia ikiwemo ya ulinzi wa kamera za CCTV, ukaweka mifumo ya viashiria moto (fire alarm systems) ukaweka milango ya umeme n. k. Hebu niambie mpangaji akija na ana uwezo wa pesa atachagua kukaa nyumba ipi? Jibu unalo.
Sasa niongee na watu wa Dodoma ambao tafsiri ya fursa kufuatia ujio wa makao makuu ya nchi wanaichanganya sana na mahitaji na viambata vya fursa hiyo.
Naomba niwakumbushe kama si kuwaekewesha ndugu zangu wa Dodoma kuwa, fursa pekee kwa sasa kubwa ni moja tu. Nayo ni "KUTANGAZWA NA KUHALALISHWA KISHERIA JIJI LA DODOMA KUWA MAKAO MAKUU YA NCHI "Hiyo Ndiyo fursa yenyewe.
Sasa inakuwa kubwa na pana kiasi cha kuonekana kumnufaisha kila mtu kwa sababu ya VIAMBATA VYAKE NA MAHITAJI YAKE.
Viambatana kwa Dodoma kutangazwa kuwa Makao makuu ya nchi ni pamoja na ONGEZEKO LA WATU HASA LA WATU WA MADARAJA FLANI -wakiwemo wafanyakazi,wawekezaji, wafanyabiashara n. k. Sasa ongezeko hilo la watu siyo hitaji la fursa ila ni kiambata cha fursa hiyo.
Hitaji linalotokana na kiambata hicho cha fursa hiyo ni pamoja na
NYUMBA ZA MAKAZI NA BIASHARA, HUDUMA ZA KIJAMII N. K. na hili eneo la uhitaji ndilo la kuchangamkia.
Zinahitajika nyumba na huduma za kijamii zenye kiwango na hadhi. Ndipo hapo ubunifu unaingia sasa. Unafahamu Mabalozi watakuwepo Dodoma, Je siku za weekend wakitaka kutoka kufurahi na familia zao maeneo ya kuwavutia na kutoshekeza yapo?
Je wakiamua watoto wao wasome shule hapa Dodoma, Je shule za hadhi ya kimataifa zipo na zinatosheleza?
Na kadhalika na kadhalika.
Dodoma mpo?
Salaam Dodoma!
Naitwa Kennedy Salvatory Festo (Dkt Kenny)
April 2,2019.
Playtech unveils latest mobile casino game - JTG Hub
ReplyDeletePlaytech 울산광역 출장샵 unveils 원주 출장샵 latest mobile 고양 출장마사지 casino game 속초 출장안마 - 제주도 출장안마 JTG Hub